Saturday, August 24, 2019

_*JINSI AMBAVYO MANENO YA KIAGANO YANAVYOWEZA KUATHIRI MAISHA YA WATU*_

```Sehemu ya 1```

Yeremia 11

1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,

2 Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu;

3 ukawaambie, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya,

Bwana Yesu asifiwe sana sana.

Agano ni _*maneno ya kimapatano kati ya Mungu na watu ,au kati ya miungu na watu na hayo maneno huwa yanasimamiwa na nguvu ya kiroho kutoka kwa Mungu kama watu wamefanya agano nae ,au kutoka kwa miungu kama watu wamefanya hayo maagano na hiyo miungu.*_

Hakuna agano pasipo na nguvu ya kiroho inayokuwa ikiambatana na hilo agano.

Ukiisha tu kulifanya agano na Mungu au na miungu ni lazima nguvu ya kiroho kutoka kwao ije juu yako ili kutimiliza vile vyote mlivyokwisha kupatana wakati mnafanya agano pamoja nao.

Na ile nguvu iliyoko ndani ya agano fulani kati yako na Mungu au na miungu ndiyo inayokwenda ikiathiri maisha yako siku hadi siku, iwe kwa mema au kwa mabaya.

Kwenye Yeremia 2:2 na 3 utaona Mungu ambaye ni Roho kuu na Takatifu sana ,akifungua kinywa chake na kuachilia nguvu ya kiroho inayoitwa laana juu ya watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; na anatueleza na sababu ya kwanini ameamua kuiachilia aina hii ya nguvu ya kiroho juu ya hawa watu.

Kwenye mstari wa 3 utaona akisema hiyo sababu na sababu ni uwepo wa maneno ya kiagano kati yao na Yeye Mungu ambaye ni Roho kuu sana na yenye nguvu kuu sana ya uumbaji wote.

Uwepo wa maneno ya kiagano ulikuwa na kipengere cha kuachiliwa kwa laana juu ya watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; laana ilitokea pale walipojikuta wameyaacha maneno ya kiagano kati yao na Mungu.

Laana ni nguvu kamili ya kiroho yenye kuleta athari kwa watu ambao agano fulani linawahusu kwa namna moja au nyingine ,kati yao na Mungu au na miungu.

Mungu anayo nguvu ya kwake inayoitwa laana na pia na Shetani anayo ya kwake inayoitwa laana na huwa wanaziachilia kwa watu pale tu watu wanapoyaacha maneno yao ya kimaagano na kufuata mengine kinyume cha agano lao.

Kinachonishangaza kwenye mstari wa 3 ni kwamba hatuoni watu wa Yuda na Yerusalemu wakiambiwa kwamba wafunge agano na Mungu ,bali utaona wakipelekewa maneno tu ,yenye kusema kwamba kila mtu asiyeyasikia maneno ya maagano atalaaniwa.

Swali la kujiuliza hayo maagano yalifanyika lini kati yao na Mungu mpaka waambiwe kuwa kama wasipoyasikiliza maneno yaliyoko ndani ya agano kati yao na Mungu watalaaniwa.

Ni mambo ya kuyatafakari kwa kina sana ,kwa sababu ukisoma kwenye hii mistari hapa;

Mithali:26.2

Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.

Utaona laana kama haina sababu ,haiwezi kumpiga mtu.

Kwa hiyo wana wa Yuda na Yerusalemu yale maneno ya kiagano ,yaliyoletwa kwao ,yalikuwa na sababu ya kwanini yaliwajia katika maisha yao, ingawa hakuna mahali tunaona wakifanya agano na Mungu kwa wazi wazi, wao kama wao.

Sikia sababu ya kwanini maneno ya kiagano yaliwajilia na kuwapata na kuachilia laana juu yao ni hii; ni kwamba baba zao walipokuwa wakifanya maagano na Mungu, yale maagano yalifanyika huku yakihusishwa na uzao wao baada yao, yalikuwa ni maagano ya kurithi ndani ya familia na koo zao, yalikwenda yakirithiwa kizazi kwa kizazi na Mungu alikuwa akiyafuatilia kama maneno ya kimapatano kati ya wazazi na uzao wa matumbo yao.

Kwa hiyo haijalishi uwe unajua au haujui, Mungu yeye alikuwa akidai na kutaka uzao wa wale wote waliofanya agano nae ,upate kusikia na kujielewa kuwa, wao sio uzao tu wa kawaida bali ni uzao wenye kufuatilia na maeno ya kimaagano yenye nguvu ya baraka na laana kwa wasiosikia na kufuata hayo maagano, na hapa ndipo penye chimbuko la kujikuta unaishi maisha magumu sana na yenye taabu sana.

Usipojua kwamba agano lipo na linakufuatilia utaishi maisha magumu sana sana ,kwa sababu hautajua sababu ya kwanini laana au kutokufanikiwa katika maisha kunakupata kila siku.

Laana isiyokuwa na sababu haina kibali cha kuendelea kukufuatilia na kukufanya usifanikiwe kila siku, kama ni laana inatokana na agano fulani lililofanyika ndani ya ukoo au familia kati ya miungu na wazee wa familia au ukoo , na lile agano lina kipengere cha kurithiwa toka kizazi hadi kizazi, ujue kwamba roho ile ya miungu itakufuatilia tu, ikitaka uwe sehemu ya kuisikia inayoyataka ya kiagano ,sawa sawa na maelewano yaliyofanyika huko nyuma ,kati ya wazazi wako na ile roho ya miungu ,waliyofanya nayo agano na haijalishi kwamba unajua au haujui ,umesikia au kwamba haukusikia, roho ya miungu itakufuatilia tu ,mpaka ujue namna ya kujitoa huko kwa msaada wa Mungu tu.

Mtu mmoja akaniuliza akasema ,mbona mimi sijawahi kushiriki mambo ya miungu ndani ya familia, sasa kwanini roho za miungu zinifuatilie katika maisha yangu.

Sikia agano la kurithi liwe la Mungu au la miungu, lenyewe likiisha kufanyika ,linatakiwa kutekelezwa bila kuachwa ,kwa hiyo kama haujui au hujawahi kuusika kabisa ,bado lina nguvu juu yako kwa sababu wewe unahesabika ni uzao wa wale waliofanya agano nao na unatakiwa urithi kila kitu cha kiagano, kiwe kizuri au kibaya toka kwao, ndio maana unafuatiliwa nao kwa nguvu kiasi cha kuathiri maisha yako.

Itaendelea 

Imeandaliwa na  Mtumishi Isaya Kakusa

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed