Thursday, March 14, 2019

FAIDA ZA KUMRUDIA MUNGU.


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.

Kama kuna kitu muhimu kwa mtu aliyekuwa amemwacha MUNGU basi ni mtu huyo kuamua kumrudia MUNGU.

Yoeli 2:12 "Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;"

Kumrudia MUNGU ni nini?

Kumrudia MUNGU ni kurudisha mahusiano na MUNGU katika KRISTO YESU.

Uhusiano huo ulikuwa umeuvunja(kwa kutokulitii Neno la MUNGU)au uhusiano huo ulikuwa hujawahi kuupata(Hujaokoka)

Ezekieli 14:6 "Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote."

Kumrudia MUNGU ni kurudi katika nafasi yako ya kwanza uliyokuwa nayo katika KRISTO.

Yeremia 18:11 "Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, BWANA asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu."

Kumrudia MUNGU ni kwenda mahali pa MUNGU ulipokuwa umepaondoka, ni kurudi katika wajibu wako kwa MUNGU.

Malaki 3:7-10 " Tokea siku za baba zenu mmegeuka upande, mkayaacha maagizo yangu, wala hamkuyashika. Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa namna gani? Je! Mwanadamu atamwibia MUNGU? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote. Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la."

Je uliacha Wokovu? Hapo ulimwacha MUNGU.

Je uliacha utumishi?

Je uliacha kutoa fungu la kumi?

Je uliacha utakatifu katika KRISTO YESU? Ndugu, hapo ulimwacha MUNGU.

Ndugu rudi kwa MUNGU katika KRISTO YESU.

Ndugu rudi katika wajibu wako kwa MUNGU.

Ndugu rudi katika utumishi wako kwa KRISTO YESU Mwokozi.

Nini kinaweza kufanyika ukimrudia MUNGU?

1. Ukimrudia MUNGU na yeye atakurudia wewe.

Zekaria 1:3-4" Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema BWANA."

Ni hatari sana kama ulikuwa umeachwa na MUNGU, ndugu mrudie MUNGU na yeye atakurudia wewe, ni faida kubwa sana ukirudiwa na MUNGU baada ya wewe kumrudia yeye katika KRISTO YESU.

2 Nyakati 30:6 "Wakaenda matarishi wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru."

2. Ukimrudia MUNGU ataghairi mabaya yaliyokuwa yamekusudiwa dhidi yako.

Yoeli 2:13" rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya."

3. Ukimrudia MUNGU atakubariki.

Yoeli 2:14 "N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu?"

4. Ukimrudia MUNGU atakuponya kama unahitaji uponyaji.

Yeremia 3:22" Rudini, enyi watoto waasi, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u BWANA, Mungu wetu."

5. Ukimrudia MUNGU utapewa iliyo haki yako.

Yeremia 35:15" Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza."

Hawa kwa kumwacha MUNGU walijikuta hata haki zao yaani kukaa katika nyumba za baba zao wanaondolewa, kumrudia MUNGU ndiko kunarudisha na haki zao.

Kumrudia MUNGU katika KRISTO YESU ni jambo la muhimu sana kwa wewe uliyekuwa umemwacha MUNGU.

Je wewe ulimwacha MUNGU kwa ajili ya nini?

Ndugu, wewe ndio unajua, Mimi kazi yangu ni kukujulisha kwamba inakupasa kumrudia MUNGU katika KRISTO YESU, rudi kwenye Wokovu, rudi kuwa mtu wa ibada, rudi katika utumishi, rudi katika wajibu wako kwa MUNGU, waambiea na familia yako wamrudia YESU, waambie marafiki zako wamrudie YESU KRISTO Mwokozi.

Mwenye sikio la kusikia naamini amesikia na sasa atamrudia MUNGU katika KRISTO YESU.

MUNGU akubariki sana kama ukifanyia kazi.

By Peter Mabula.

Mtenda kazi katika shamba la MUNGU.

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed