Wednesday, October 01, 2014

MV MAGOGONI YASHINDWA KUTIA NANGA. YAPOTEZA UELEKEO NA KUELEKEA ZANZIBAR

  • MWANAFUNZI MMOJA AZIMIA
  • ABIRIA WACHANGANYIKIWA
  • WAWAPIGIA SIMU NDUGU ZAO KUTAFUTA MSAADA

Siku ya jana tarehe 30/09/2014 majira ya asubuhi, kivuko cha siku nyingi cha MV Magogoni kiliwaweka watu wengi, hasa abiria waliokuwamo ndani ya kivuko hicho katika tafrani kubwa na sintofahamu, baada ya kushindwa kutia nanga na kuwapa abiria wasaa wa kushuka na kuendelea na majukumu yao ya kila siku ikiwemo kujitafutia ridhiki.

Kivuko kilipokaribia kutia nanga, kilijikuta kinamshinda nahodha, na kujikuta anaenda uelekeo wa Zanzibar pasi kuwa na ridhaa ya kwenda huko. Hapo ndipo abiria wengi wakaanza kupiga
 mayowe huku wengine wakiwapigia simu ndugu zao wakiomba msaada.

Kivuko hicho kilienda kombo hadi kufika kwenye mitumbwi ya wavuvi, iliyo karibu na soko la "ferry". Baada ya jitihada nyingi kufanyika kivuko kilifanikiwa kutia nanga na watu kushuka huku wakiwa wamegubikwa na hofu kubwa iliyotanda ndani 

ya mioyo yao.

|Aidha, mwanafunzi mmoja, binti, alipoteza fahamu na kuzimia baada ya kupata mshituko uliotokana na kivuko hicho kwenda kombo kwa muda wa takribani nusu saa. Lakini, hadi abiria wanashuka katika kivuko, haukujulikana mpango wowote uliofanyika kumpa msaada wa kitabibu huyo mwanafunzi.

Baada ya abiria kushuka kwa taabu iliyotokana na msukosuko uliotokea majini, wataalamu walishirikiana na baadae kupiga mbizi na kutoa uchafu uliokuwemo katika injini na hivyo kukiwezesha kivuko kuendelea na shughuli zake bila tatizo hilo kujiokeza tena.

Wakati hayo yote yanatokea, kivuko kingine kinachofanya kazi ya kuvusha watu kutoka eneo la Magogoni hadi Kigamboni ambacho hivi karibuni kimetoka katika matengenezo, MV Kigamboni, kilikiwa kinafanya kazi yake vizuri ya kuwavusha abiria, kikiwa imara na kasi maradufu ya kivuko cha MV Magogoni.

Wakati wa jioni, baadhi ya wananchi walikosa imani na MV Magogoni, baada ya kukataa kukipanda na kusubiria kupanda kivuko cha MV Kigamboni. Lakini muda mfupi, baada ya kuondoka MV Magogoni, Askari kanzu mmoja aliyevaa shati la mikono mifupi, na kusikika akiongea lafudhi ya Kihaya, alionekana akiwakomoa abiria waliokataa kupanda MV Magogoni kwa kuwakatalia katu katu kupanda MV Kigamboni, kilichokuwa kinaelekea Kigamboni. Alipoulizwa ni kwanini amefanya hivyo, akajibu kuwa kuna gari ndani ya kivuko ambalo linakijaza mafuta, hivyo hawapaswi kupanda. Kivuko kilivusha magari, ilhali kikiwa kimebeba magari mengi yaliyofurika ndani yake.

Kivuko cha MV Kigamboni, kilirudi mapema kabla ya MV Magogoni na kuruhusiwa kubeba abiria, 

baaada ya zoezi la ujazaji wa mafuta kukamilika.

Kutokana na matatizo mbalimbali wanayopata watu wanaotumia kivuko, ni wakati muafaka kwa Serikali na wananchi kwa ujumla, kuona kuwa zinahitajika jitihada za makusudi kushughulikia suala hili, ili yasije yakatokea maafa ambayo yataigharimu serikali mamilioni ya shilingi kuliko ingelishughulikia suala hili mapema. Tukumbuke kuwa "usipoziba ufa, utajenga ukuta".
Picha kwa hisani ya "michuzijr2.wordpress.com"

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed