Sunday, September 07, 2014

HEKIMA YA KUJIBU MASWALI

 Askofu Zachary Kakobe

Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 21:23-46. Ingawa somo letu ni “HEKIMA YA KUJIBU MASWALI”, hata hivyo, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii. Katika mistari hii, tunapata mambo manne tofauti, ya kujifunza:-

(1)HEKIMA YA KUJIBU MASWALI (MST. 23-27);

(2)UBATIZO UNATOKA MBINGUNI (MST. 25-27);

(3)NEEMA INAYOAMBATANA NA KUTUBU (MST. 28-32);

(4)MFANO WA MTU MWENYE NYUMBA (MST. 35-46).


(1) HEKIMA YA KUJIBU MASWALI (MST. 23-27)

Yesu Kristo, alikuwa na hekima ya kipekee katika kujibu maswali aliyokuwa anaulizwa kiasi ya kwamba watu hawakuthubutu kumwuliza maswali (MATHAYO 22:46). Hatupaswi kujibu kila swali tunaloulizwa, kwa mfumo uleule. Maswali mengine hayahitaji majibu yetu kabisa (YOHANA 19:8-9; MATHAYO 27:12-14), na majibu ya maswali mengine, ni kuwauliza maswali hao waliotuuliza (MATHAYO 21:23-27). Kabla ya kujua hatua ya kuchukua tunapokabiliwa na swali, ni muhimu kwanza kuifahamu NIA ya swali lile tuliloulizwa, na pia aina ya swali lile. Maswali tunayoulizwa, yako katika namna sita zifuatazo:-

a. MASWALI YA MTEGO (MATHAYO 22:15-17) – Ni muhimu kujihadhari katika kujibu maswali ya jinsi hii, ili kujibu kwetu kusitufanye tunaswe katika mtego tuliowekewa na mtu anayeuliza swali.

b. MASWALI YENYE NIA YA KUTUJARIBU (MATHAYO 19:3; LUKA 10:25) – Maswali haya huwa yana lengo la kutujaribu ufahamu wetu, kutujaribu kwamba tutajibu namna gani, ili anayeuliza swali, apate nafasi ya kutulaumu, kutushtaki au kupeleka taarifa mbaya mahali fulani. Inahitajika tahadhari katika kujibu maswali haya.

c. MASWALI YENYE NIA YA KULETA MADHARA (MATHAYO 2:3-8) – Kwa kutoa jibu kamili la maswali ya jinsi hii, tunaweza tukampa mtu yule aliyetuuliza, nafasi ya kufanya madhara aliyoyakusudia moyoni. Mwizi anaweza kuuliza, Je, mtu huyu huwa anarudi jioni kutoka kazini kila siku? Nikija asubuhi ni vigumu kumkuta? Nyumbani kwake hakuna yeyote anayebaki? Inahitajika tahadhari katika kujibu maswali ya namna hii. Maswali ya kuleta shari, pia hatupaswi kuyajibu.

d. MASWALI YENYE NIA YA KUJIDAI (LUKA 10:29) – watu wengine, siyo kwamba wanauliza kwa kutaka kuelimishwa, la, hasha. Wao wanajidai kwamba ni wenye elimu kutupita na hivyo wanauliza maswali ili kutafuta kosa kwetu, halafu wao watuonyeshe kujua kwao. Inatupasa kuwa na tahadhari. Tusijibu maswali kwa nia ya kutafuta mashindano ya “Nani anajua zaidi”, tutafute zaidi kujibu maswali ya kumfanya mtu aache uovu. Kujibu swali la maana ya vitasa, mihuri na baragumu za Ufunuo wa Yohana kutoka kwa mtu ambaye hajaookoka au ambaye hajaishi sawasawa na misingi ya Utakatifu, ni kupoteza muda wetu bure (2 TIMOTHEO 2:14, 16-18).

e. MASWALI YA UPUMBAVU NA UPUUZI, YASIYO NA ELIMU (2 TIMOTHEO 2:23; TITO 3:9)  Maswali yoyote ya kuzua ugomvi au majadilianao ya kipuuzi tunapaswa kuwa mbali nayo. Tunapokuwa tunawashuhudia watu habari ya wokovu, tuepuke maswali yao yanayohusiana na mafundisho ya ndani – Utatu wa Mungu, Uwana wa Mungu, Malipizo ya Ndoa, Mavazi ya mtu aliyeokoka, Ubatizo n.k. Tuwaeleze tu njia ya kushinda dhambi na kukwepa maswali mengine. Watafahamu hayo BAADA ya kuokoka. Mtu haanzi darasa la saba, anaanzia darasa la kwanza. Maswali ya upuuzi kama “Mungu alitokea wapi”, n.k., tuyakatae. Kabla ya mtu kujua Mungu ametokea wapi, ajifahamu kwanza yeye ametokea wapi!

f. MASWALI YENYE NIA YA KUJIFUNZA (MATHAYO 19:25-29; LUKA 20:27-37) – Maswali haya yana nia njema, hata hivyo, inatubidi kuangalia kwanza kiwango cha kiroho cha mtu. Mtoto mdogo wa miaka mitano akiuliza “watoto wanatoka wapi?”, huwezi kumjibu kwamba wanatokana na tendo la ndoa! Kufanya hivyo ni kumpeleka mbali na maadili safi. Vivyo hivyo, watoto wachanga kiroho, tuwajibu maswali ya kuwajenga tu katika uchanga wao. Tuwape maziwa, na kamwe, tusiwape mifupa (WAEBRANIA 5:12-14; 1 PETRO 2:2).


JINSI YA KUPATA HEKIMA YA KUJIBU MASWALI – Inahitajika hekima ya Mungu katika kujibu Maswali. Tukiipata hekima hii, tutafahamu upesi nia ya swali na kujua jinsi ya kulikabili swali hilo mara moja. Hekima hii inapatikana kwa kuiomba kwa Mungu kwa imani kwamba atatupa, ili tumtumikie vema (YAKOBO 1:5-7).

(2) UBATIZO UNATOKA MBINGUNI (MST. 25-27)

Katika mistari hii, tunajifunza waziwazi kwamba, Ubatizo wa Yohana, ulitoka mbinguni, na siyo kwa wanadamu. Ndiyo maana wakuu wa makuhani na wazee wa watu waliogopa kumjibu maana hawakumwamini Yohana, ingawa watu wote walimwona kuwa ni nabii. Ikiwa Ubatizo wa Yohana, ulitoka mbinguni, ni dhahiri kwamba Ubatizo wa Yesu aliye mkuu kuliko Yohana (YOHANA 1:28-30), ULITOKA MBINGUNI NA SIYO KWA WANADAMU (YOHANA 3:26-27). Kwa kuwa ubatizo huu wa maji tumeagizwa kubatizwa na aliyetupa agizo hilo ni Yesu mwenyewe (MATHAYO 28:19; MARKO 16:15-16), na siyo mwanadamu hatupaswi kukubaliana na mafundisho ya wanadamu kuhusiana na Ubatizo. Yesu kamwe hakuagiza watoto wadogo wabatizwe. Yeye hakubatizwa utotoni, bali alibarikiwa, na katika utumishi wake, aliwabariki watoto, hakuwabatiza (LUKA 2:27-35; MARKO 10:13-16), Yesu alibatizwa akiwa mtu mzima (LUKA 3:21-23). Ubatizo huu uliotoka mbinguni, unafanyikaje? Neno “kubatiza”, kwa lugha ya asili ya kiyunani, linaitwa “BAPTIDZO”, linatokana na neno la kiyunani “BAPTO” lenye maana ya “KUZAMISHA” au “KUCHOVYA”, kama kuchovya tonge la ugali kwenye mchuzi au kuchovya nguo katika maji au damu, au kuchovya ncha ya kidole katika maji (LUKA 16:24; UFUNUO 19:13; YOHANA 13:26). Hivyo, ubatizo uliotoka mbinguni, unafanyika kwa kumzamisha mtu katika MAJI TELE yanayomfunika mtu (YOHANA 3:23) na siyo kunyunyizia maji usoni. Vilevile, Ubatizo uliotoka mbinguni, unafanyika BAADA (siyo kabla) ya mtu kusikia mahubiri ya Injili na kuiamini, na kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, na kuamua kuokolewa (WARUMI 10:13-14; MATENDO 8:12, 36-39). Ni katika maji tele tu, mtu anapoweza kutelemka majini na kupanda majini (MATHAYO 3:16; YOHANA 4:1-2; LUKA 2:27-35; MARKO 10:13-16).

(3) NEEMA INAYOAMBATANA NA KUTUBU (MST. 28-32)

Mungu anapendezwa na watu walio tayari kutubu au kuungama na KUACHA yale waliyokuwa wakiyafanya, na kuanza kufanya yale ambayo walikuwa hawataki kuyafanya. Watu wa namna hii, wanapata rehema au neema ya kuwawezesha kushinda dhambi, na kupata haki ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13). Wako watu wengine ambao hawako tayari kutubu, wanajikinai, na kujiona, ni wenye haki, kwa kuwa hawanywi pombe, hawavuti sigara, hawafanyi uasherati, hawaibi, na wanafanya taratibu zote za kidini. Hawa watakwenda mtoni, na kuzidiwa na watoza ushuru na makahaba walio tayari kutubu na kuacha. Namna yoyote ya mtu kujiona hana hatia, ni machukizo mbele za Mungu, maana kwa kuzaliwa, kila mtu ni mwenye dhambi, hivyo kutubu ni lazima ili kukwepa hukumu (YEREMIA 2:35; 1 YOHANA 1:8-10; WARUMI 3:12, 22-23). Hata mtu akiwa ni mwenye dhambi kiasi gani kama kahaba, akitubu kwa kumaanisha kuacha, anasamehewa na kuokolewa (ISAYA 1:18; 55:6-7). Vilevile, ni muhimu kuwa tayari kutubu hata baada ya kuokolewa. Baada ya kuokolewa na hata baada ya kutakaswa pia, bado tutaandamwa na DHAMBI ZA KUTOKUTENDA YANAYOTUPASA KUYATENDA (YAKOBO 4:17). Ni lazima tuwe na utayari wa kutubu wakati wote kama Daudi (1 NYAKATI 21:1, 7-8; 1 YOHANA 2:1-2)

(4) MFANO WA MTU MWENYE NYUMBA (MST. 33-46)

Mtu mwenye nyumba, alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo. Mashamba ya mizabibu yalizungushiwa ugo au boma au ukuta wa mawe (MITHALI 24:30-31). Akachimba shimo la shinikizo ndani yake. Shimo la shinikizo, ni mtambo wa kukamua juisi kutoka katika zabibu. Zabibu huwekwa upande mmoja wa mtambo, maganda yake huangukia shimoni na juisi hupita upande wa pili. Akapangisha wakulima, akasafiri. Wakulima walipewa mashamba haya kwa kuyakodi kwa mwaka au maisha na pia walipewa kwa urithi. Mtu mwenye nyumba hapa, ni Mungu mwenyewe (1 WAKORINTHO 3:9; WAEBRANIA 3:2,6). Shamba hili la mizabibu, ni Kanisa la jangwani ambalo walirithishwa Wayahudi peke yao na lilikuwa na ukuta, hakuna mtu ambaye siye Myahudi aliyeruhusiwa kuingia katika Kanisa hilo. Mungu alituma watumwa wake yaani MANABII wake, kutaka matunda kwa Wayahudi. Wayahudi, waliwakamata, kuwapiga kwa mawe na kuwaua (MATHAYO 23:34-37). Hatimaye Mungu akaamua kumtuma Mwanawe Yesu akisema watamstahi. Naye wakamtesa nje ya lango na kumwua. Kwa sababu hiyo, Kanisa sasa litarithishwa au watapewa Mataifa na ukuta wa kutokuwaruhusu kuingia, hautakuwapo (MATENDO 13:46-49; 15:13-18). Yesu ni Jiwe kuu la pembeni. Yeyote aangukaye juu yake, atavunjika-vunjika. Neema yake itamfanya awe na moyo uliovunjika na kupondeka, na hivyo kuokolewa (ZABURI 34:18; 51:17; 147:3). Bali wale watakaomkataa; wataangukiwa na Jiwe hilo na kusagwa tikitiki kwa kuvunjwa vipandevipande na kuangamizwa (ISAYA 8:9; MATENDO 7:38).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe


source: http://davidcarol719.wordpress.com

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed