Sunday, October 27, 2013

SIRI ZA ASKOFU KAKOBE


Taja jina ASKOFU KAKOBE popote Tanzania na utashangaa kujua kwamba karibu kila mtu anamfahamu. Wengi walimfahamu pale alipoweka historia ya kujitosa katika ulingo wa siasa na kumpigia debe Augustino Lyatonga Mrema. Hiyo ilikuwa ni mwaka 2000 wakati wa uchaguzi mkuu. Mengi yalisemwa kumhusu, lakini mimi naheshimu uhuru wake kama mtanzania kutangaza msimamo wake kisiasa katika nchi yake. Tena kama Askofu anaeongoza kanisa la Full Gospel Bible Felloship alikuwa na haki kuwatangazia washirika wake ambao pia ni wanachama wa vyama tofauti vya kisiasa msimamo wake kisiasa kama kiongozi wao kidini. Kwangu kama kuna wakati niliwahi kumheshimu Kakobe basi ni wakati huo. Aliwakemea waziwazi bila woga CCM Chama Cha Majambazi na kuvumilia vishindo na matisho yao. Japo kwa sasa hana misimamo mikali kuihusu CCM hiyo inaeleweka. Nani aipinge CCM aishi salama Tanzania? Kama hawatakuua, basi watakufuatilia kila ufanyalo na kabla ujue kila kitu kwako kitakuwa kichungu. Nasikia Kakobe walimfuatilia kiasi cha kulisambaratisha kanisa lake. Kila neno baya waliloweza kulisema kumhusu basi walilisema. Kila mbinu chafu ya kisiasa CCM waliyoweza kuitumia kinyume cha Mtumishi wa Mungu Kakobe basi waliitumia mradi tu waone kwamba walimharibia katika kila jambo. Hata kama Kakobe leo amepunguza misimamo mikali kuhusu CCM, lakini mimi namwita shujaa alieandika historia ya watumishi wa Mungu walioipinga CCM mchana jua linawaka. Kwa hilo Kakobe ni mfano wa kuigwa.


Lakini Kakobe ni nani hasa? Je tunamfahamu kweli KAKOBE? Nini kinachomfanya awe alivyo? Mimi mwinjilisti na mwimbaji wa nyimbo za injili, Faustin S. Munishi nakuletea Kakobe ambaye hukuwahi kumfahamu. Tulifahamiana naye kwenye miaka ya themanini hadi mwaka 84 nilipohamia Kenya na kumwacha Kakobe Tanzania. Kwa miaka niliyomfahamu, huyu ndiye Kakobe Zakaria Mokovu jeuri anayejiamini katika kila afanyalo. Wengi huchanganya bidii ya mtu katika kile akifanyacho na upako wa kiungu. Cocacola imafanikiwa kuuzwa duniani kote siyo kwamba wenye kampuni wameokoka, bali ni juhudi zao katika kutangaza bidhaa yao. Biashara nyingi duniani zimefanikiwa kwa wenye biashara hizo kufuata kanuni za biashara. Mengi hajawahi kusema kama ameokoka au la, lakini kibiashara bado anaongoza. Je Kakobe huendesha kanisa akitumia kanuni za kibiashara? au anatumia kanuni za neno la Mungu?

Alianza kama mmachinga wa kunakili nyimbo za wasanii mbali mbali bila kibali kutoka wasanii hao. Ingekuwa ni wakati wa sasa angekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kunakili nyimbo bila kibali cha wasanii, lakini wakati huo alipewa leseni ya kufanya kazi hiyo. Cha ajabu aliitangaza kazi hiyo haramu kwenye vyombo vya habari. Jina la kampuni yake lilijulikana kama MULANGA EDITION. Hiyo ilikuwa kwenye miaka ya themanini. Bidii yake ya kujitangaza, na kuamini alichokifanya hata kama ni kazi haramu, zilimfanya ajulikane Tanzania nzima kama mnakili kanda maarufu. Sishangai watu wanaposema kwamba kanisa analoliongoza la Full Gospel Bible Felloship ndilo linaloongoza makanisa ya Kipentekoste kwa idadi ya watu. Lakini hiyo haimaanishi kwamba kanisa hilo ndilo kipimo cha makanisa Tanzania kwani hata wengi mara nyingi hukosea. Ila nisieleweke kama ninayesema kwamba kanisa la Kakobe siyo la kweli, lakini siwezi pia mia kwa mia kusema kinyume chake. Mungu pekee ndiye mwenye kipimo cha kuhukumu kanisa gani la kweli. ILa siyo vibaya watumishi wa Mungu wakitoa tadhimini yao kuhusu yale wanayoyaona na kuyasikia, na kwa sababu wana roho wa Mungu ndani yao, mara nyingi hawatakosea sana. Nisemayo nayasema kama mtumishi wa Mungu. Pengine niseme kwamba mimi ni mtumishi wa Mungu. Ninajiamini hivyo. ila simzuii mwingine kuniona vinginevyo kwani hata ninayemsema hapa pengine naye anajiamini ni mtumishi wa Mungu.

Pengine Askofu Kakobe atakuwa amesahau, lakini mimi siwezi sahau. Nyakati hizo tulikuwa tukikutana mara nyingi na kujadili mengi yanayohusu wokovu na kukua kwa kanisa la Mungu kwa ujumla. Kwa muda wote tuliowahi kujadili mambo na Kakobe, nilimchukulia kama mtu aliyekuwa na upeo mkubwa wa kuchambua mambo na hakuwa mtu rahisi wa kufuata mambo kama bendera ifuatavyo upepo. Mara nyingi alihoji kuhusu pesa walizokuwa wakichanga kwa maandalizi ya mikutano ya Mwinjilisti Kulola, aliwahi kuniambia kwamba mikutano hiyo inaanza kukosa maana na inaelekea kugeuzwa kama sherehe za kila mwaka. Kwa mtazamo wake wakati huo, Lengo zima la kuwaleta wenye dhambi kwa Yesu lilikuwa linasahaulika na badala yake washirika wa makanisa ambao tayari walikuwa wamemwamini Yesu, ndio waliokuwa wakija kusheherekea injili. Wakati huo nilikubaliana naye mia kwa mia japo nilikuwa nikizunguka mikoa yote Tanzania na mwinjilisti Kulola. Kama Kakobe angeitisha mapinduzi wakati huo, tungeungana kumpindua Kulola. Lakini yale aliyokuwa akimlaumu Kulola kwayo, sijui kama wengine wakimlaumu yeye sasa atasemaje. Lakini Kakobe hakosi la kusema kama nimjuavyo. Pamoja na kwamba hakuwa tajiri wa kutisha kama alivyo sasa, Kakobe Alijiamini, alijipenda sana. Isingekuwa ajabu kumuona Kakobe na mke wake pamoja na mtoto wao wa kwanza wakitembea kwa miguu katika barabara ya Samora siku ya Jumapili baada ya ibada. Mara nyingi tulikutana mjini bila taarifa wala kujiandikisha na tulijadili mengi mimi na Kakobe. Miaka imepita na mengi yamebadilika. Sitarajii sasa kumpata Kakobe akila mhogo wa kuchoma pale Kariakoo, Lakini asishangae akinipata pale Kariakoo kwa mama ntilie nikila wali nusu sahani na kisamvu. Ndiyo maisha yangu. Bado niko huru kama alivyokuwa Kakobe miaka ya themanini.


Alikuwa mtu huru. Watu waliijua MULANGA EDITION kuliko mmiliki wake ambaye alikuwa Kakobe, Jambo lililomfanya huru kutembea kona zote Dar bila watu kuanza kuonyeshana Kakobe ndiye yuleee. Nina mashaka kama sasa akiwa askofu mkuu anaweza kudhubutu kutembea huru kwenye barabara za Dar. Kwa sasa watu wanamjua Kakobe kuliko kanisa la Full Gospel Bible Felloship, analoliongoza kama askofu mkuu. Pia mwenyewe sidhani kama atapenda kuonekana mjini akiwa bila gari kubwa, itakuwa kujidhalilisha. Lakini mimi bado niko huru kutembea kona zile tulizokuwa tukikutana miaka ya themanini, na sitokubali chochote kininyanganye uhuru huo. Siyo umaarufu au sifa za wanadamu zinazoweza kuninyanganya uhuru wa kukutana na watu, na kwenda nitakako kwa wakati nitakao. Kama cheo ndicho kinachoweza kusimama kati ya mimi na uhuru wangu, basi najua nitakavyofanya. Tuache hayo ya mimi, tuendelee na yake Kakobe.

Pamoja na biashara yake ya MULANGA EDITION ambayo ilikuwa inashamiri kila kukicha, Kakobe alikuwa mshirika mtegemewa wa kanisa la TAG Temeke. Alitegemewa sana kanisani hapo kwa michango ya kila aina kanisani. Kama ilivyokuwa kawaida ya makanisa mengi ya Kipentekoste nyakati hizo, wengi kati ya washirika walikuwa hoi kimaisha, jambo lililowafanya wachache waliojiweza kubeba mzigo wote wa mahitaji ya kanisa. Kakobe wakati huo alikuwa anajiweza kimaisha jambo lililomfanya awe na uhusiano wa karibu sana na Mchungaji. Mchungaji wa kanisa la Temeke wakati huo alikuwa ni Masalu. Kakobe mara nyingi alikuwa akilalamika kuhusu michango isiyoisha kanisani, na hasa akitilia maanani kwamba yeye na wenzake wachache ndio waliokuwa wakibeba mzigo huo. Siku moja aliwahi kunihoji wakati wa moja ya mikutano ya Mwinjilisti Moses Kulola, na ilikuwa kuhusu mahali nilipopangiwa kulala na aina ya chakula nilichokuwa nikipewa wakati wote wa mkutano huo. Nilipomweleza kwamba nilikuwa nakula chakula cha kawaida yaani maharagwe na ugali au na wali, alionyesha kutolifurahia hilo. Japo hakuwa na cheo chochote kanisani, aliniahidi kwamba ataongea na mchungaji na watanihudumia kama mtumishi wa Mungu mwalikwa. Kweli jioni iliyofuatia chakula changu kilibadilishwa na nikawa nakula sawa na Mwinjilisti Moses Kulola tena kwenye meza moja. Itakumbukwa kwamba kwenye mkutano huo nilikuwa mhudumu kwa njia ya uimbaji. Kwamba Kakobe alikuwa akirekodi nyimbo zangu na kuwauzia washirika huo ni ukweli usiopingika. Lakini heshima aliyoionyesha kwangu wakati huo ilikuwa siyo ya kawaida. Pengine ilikuwa ni kutokana na biashara yake ya kunakili nyimbo za waimbaji mbalimbali, ndiyo iliyomfanya awaheshimu wasanii wote kwa ujumla sijui. Lakini bila kuongeza chumvi Kakobe alikuwa mtu pekee kuwahi kuipa heshima ya hali ya juu huduma yangu ya uinjilisti kwa njia ya uimbaji, wakati waimbaji walichukuliwa si lolote kanisani. Ila siwezi kujua kama bado anawaheshimu wasanii wakati huu akiwa Askofu mkuu.

Majuzi nilipata nafasi ya kulitembelea kanisa lake la Full Gospel Bible Felloship jijini Dar es Salaam. Kulikuwa na kongamano la wachungaji zaidi ya 8000 wa makanisa mbali mbali ya kipentekoste. Ni kitambo kidogo tangu tukutane na Kakobe uso kwa uso. Tangu miaka ya themanini hadi themanini na nne sikumbuki kama tumewahi kukutana. Ukizingatia kwamba miaka mingi hatujaonana na mtumishi wa Mungu Kakobe, halafu uchanganye na Mengi tuliyowahi kujadili na Kakobe kuhusu Kanisa la kipentekoste Tanzania na Hatma yake, Tena uongeze na Askofu Kulola ambaye miaka hiyo alikuwa na vita kali kati yake na Askofu Emanuel Lazaro, na wote wako kwenye kongamano, Kwa nini mimi Munishi nisiwepo? Hata kama siyo kuhudumu kama mwimbaji, nikae nisikilize wasemavyo wengine. Kwa kuwa ilitokea kwamba niko Dar kwa kipindi hicho, na kuna mkutano wa kihistoria kama huo, ningeukosa basi sijui mimi ningekuwa mhubiri wa jinsi gani nisiyefuatilia matukio ya kiinjili katika nchi yangu Tanzania.

Sikuruhusiwa kuingia kwenye mkutano huo kwa kile walichokiita kukosa kadi maalum kuniwezesha kuingia. Pamoja na jitihada zangu kutaka nipelekwe mahali pa kujiandikisha niipate kadi hiyo, lakini walinzi baada kwenda jukwaa kuu kupeleka suala langu walirudi na kunibeba juu kwa juu kunitoa kwenye mlango wa kuingilia mkutanoni na mlango kufungwa. Nilipojaribu kujieleza kwamba lengo langu ni kumsikiliza Askofu Kulola ambaye alikuwa anahubiri kwa wakati huo, majibu yalikuwa kwamba "Hii siyo injili ya kawaida. Ingekuwa hivyo tungeiweka viwanja vya JANGWANI." Siwezi kuwalaumu walinzi mlangoni kwa maswahibu yaliyonikuta, kama kulaumu nitamlaumu Kakobe mwenyewe. Ila kimahusiano mema, Kakobe atawalaumu walinzi kwa kunitimua mkutanoni. Lakini mimi najua walinzi walikuwa wakitimiza maagizo ya BOSS wao Kakobe. Ila sina kinyongo, Kanisa ni la Kakobe, walionizuia kuingia ni walinzi wa Kakobe, sasa wa kulaumu lazima awe Kakobe. Ingekuwa Kanisa ni la Yesu kama inavyostahili kuwa, basi hakuna mwenye mamlaka ya kunitimua hapo. Tena kanisa la Yesu linapaswa kuwa la jumuia na siyo mali ya mtu. Katika nyakati tulizo nazo ambapo makanisa yanabinafsishwa na kuwa mali za watu binafsi, basi wengi watatimuliwa kama mimi. Wananicheka kwa sababu nimeanza kutimuliwa, lakini ukimuona mwenzio ananyolewa, kichwa weka maji kwani wakimaliza na huyo itakuja zamu ni yako.

Baadaye ndipo nilipokuja kuelewa kwamba Lengo la mkutano lilikuwa ni kuweka mikakati ya kujenga mahusiano mazuri kati ya kanisa na serikali. Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa umoja huo Askofu Sylvester Gamanywa alisema, wakati umefika kwa serikali kutowapuuza wapentekoste. Alidai kwamba wapentekoste hawapewi nafasi katika vyombo vya habari vya kitaifa jambo ambalo alisema limechangiwa na dhana potovu kwamba walokole ni watu waliochanganyikiwa kimaisha na hawana lolote la kuweza kuisaidia serikali kiutawala. Naye Askofu Kitonga wa kanisa la Redeemed Kenya alisema anaunga mkono kongamano hilo na akasema anafurahi kuona askofu Kakobe akiufuata ushauri wake wa kutoipinga serikali iliyoko madarakani. Aliongeza kwamba nchini Kenya serikali iliyokuwa madarakani ilitambua umuhimu wa wapentekoste na iliwatumia sana katika kuwasilisha sera za serikali kwa wananchi ambao wengi ni washirika wa makanisa hayo....
source:
maelezo: http://www.gospelgtv.com, picha: http://samsasali.blogspot.com

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed