Thursday, January 03, 2013

BISHOP MWASOTA AONYA KUHUSU ‘COPY’ KATIKA UKRISTO.Bishop David Mwasota wa kanisa la Naioth Gospel Assembly lililopo mabibo external, Dar es salaam amesema hayo katika ibada ya kuanza mwaka mpya wa 2013 hapo kanisani ambapo washirika wemgi walijitokeza katika madhabahu ya Bwana na kutoa shuhuda kwa mambo Mungu aliyowafanyia kwa mwaka mzima wa 2012.

Akionya katika mahubiri yake alisema kwamba hivi sasa kumezuka imani katika Ukristo ambazo waumini hufanywa kumfikia Mungu kupitia watumishi wanaowaongoza. Watumishi hawa huwafanya waumini wao kuwategemea wao kwa mambo yote ya kiroho hususani suala zima la maombi na hivyo kuwafanya wasiwe na uwezo wa kujitegemea kiroho.

Bishop Mwasota aliweka bayana kuwa hali hii ni ‘copy’ nyingine iliyokuja badala ya imani ile ambayo wengi walikuwa nayo awali kabla ya kuokoka ambapo waumini humwendea Mungu kupitia kwa watumishi. Askofu alisisitiza hili akitolea mfano kwa watumishi wengine wanaosisitiza watu kwenda kwao kuombewa tu pasi na kuwahimiza kufanya mambo mengine yawapasayo kufanya.

Aidha, Askofu Mwasota ambaye ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (PCT), alifanya maombi ya kifamilia kwa washirika wake katika ibada hiyo pamoja na kuombea mafuta ya mizeituni ambayo waumini walikuja nayo ili yawe na upako utakaosambaratisha matatizo na nira katika maisha yao. Askofu ameamua kuweka upako katika mafuta na waumini kuyatumia kupaka kichwani, katika nyumba n.k. baada ya yeye kupata muujiza mkubwa kutokana na mafuta yenye upako.

Mbali na hayo, katika ibada hiyo Mtumishi wa Mungu alitamka baraka kwa washirika ikiwa pamoja na magari na fedha nyingi kwa mwaka 2013. Baada ya yote, siku iliisha kwa kula chakula cha pamoja kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya wa 2013 ambapo watu wa rika zote, wake kwa waume walishiriki katika chakula hicho.


(picha kwa hisani ya blogu ya gospelkitaa)

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed