Wednesday, May 09, 2012

MCHAKATO WA KUTAFUTA KATIBA MPYA: WAKRISTO IMEWAPASA KUWA MACHO.


Rais Bashir wa Sudan ambaye nchi yake ni miongoni mwa nchi zinazotukuza uislam na kuwanyanyasa Wakristo waishio nhini humo


Na Mwandishi wetu
Wakristo kote nchini Tanzania wanahimizwa kuwa na macho na mchakato mpya wa katiba inayotarajiwa kuletwa kutokana na michango ya wadau wa kada mbalimbali nchini wao wakiwemo katika mjumuisho.

Aidha wanahimizwa kuwa tayari kutoa maoni yao kuhusu aina ya katiba wanayohitaji kuwa nayo ili kuendeleza lengo, nia na dhumuni lao la kumwabudu Mungu wao na kuwahimiza watu wengine kumfuata Bwana Yesu Kristo na kuepukana na maovu katika siku hizi za mwisho.

Umuhimu wa Wakristo katika kuchangia mawazo katika katiba mpya ni dhahiri kwani itawawezesha wao kupata katiba inayowawezesha kuwa na uhuru wa kuabudu katika imani yao bila ya kuingiliwa na mtu yeyote kwani kuna nchi nyingine barani Afrika na duniani kwa ujumla ambazo uhuru wa kuabudu kwa waumini wa dini za Kikristo ni ndoto.
 
Tukianzia hapa barani Afrika; katika nchi ya Somalia kuna upinzani mkali usioelezeka kuhusu imani ya Kikristo na watu wengi wamejikuta wakiuawa na kupoteza maisha yao pindi wanapogundulika kuwa wao ni Wakristo. Haya yalitanabaishwa na mhubiri maarufu wa kisomali anayeitwa Adam Haji Mohammed ambaye ni msomi aliyepata shahada ya sheria na kufuzu mafunzo ya juu katika dini ya kiislam kabla hajampokea Yesu kuwa Mwokozi wa maisha yake. Mtumishi huyu anaeleza kuwa waumini wake kadhaa waliuawa alipokuwa huko nchini kwao Somalia kwa sababu tu ya kile kinachoitwa na Wasomali ambao wengi wao wana msimamo mkali kuhusu dini ya kiislamu kuwa ni kujiunga na dini ya makafiri.

Alisema kuwa mama yake ambaye alikubali kuokoka aliuawa na yeye kuambiwa kuuzika mwili uliokatwa vipande vipande ndani ya kiroba. Alielezea mengi ambayo katika CD za mahubiri yake ameweka mambo wazi kuhusu ushuhuda wake. Pia katika semina zake zilizofanyika katika makanisa ya jijini Dar es salaam alihubiri mambo mbalimbali ikiwemo kuelezea ushuhuda wake alipokuwa Somalia.
Pia katika nchi ya Sudan ambapo kitendo cha kuonekana ni Mkristo mtu hudharauliwa na kuonwa kuwa si kitu, imani ya Kikristo haipewi nafasi kwa wafuasi wake kutekeleza ibada zao kwa uhuru. Mambo haya yalisemwa na Mtumishi aitwaye Bukuku ambaye mwaka huu kwenye ibada katika kanisa la EAGT Kimanga linaoongozwa na Mchungaji Joseph Marego alipewa nafasi ya kutoa mahubiri.

Alisema kuwa pindi alipokuwa Somalia kwa ajili ya kulinda amani katika jimbo la Darfur, wanajeshi wa Kitanzania wengi Wakristo walilazimika wabadilishe majina yao ya Kikristo na kujipachka majina ya kiislam ili kuepuka kunyanyaswa na kubaguliwa na watu wa Sudan.

Alitanabaisha kuwa yeye hakukubali kubadilisha jina like le kwanza la Kikiristo na kupuuza hofu yeyote ya kudharaliwa wala kufanyiwa kitu chochote kibaya. Alikaa huko kwa kipindi chote na hatimaye kurudi nyumbani akiwa salama.

Kutokana na mambo kama haya inatubidi sisi Wakristo wa Tanzania kusimamia kidete kuwa na katiba itakayotupa uhuru wetu wa kuabudu ili tusiwe na ugumu na matatizo lukuki kama yaliyo katika nchi hizi mbili ambapo kuna nchi nyingine nyingi ambazo sijazitaja kama Iraki na Saudia ambazo Mkristo huwa katika wakati mgumu kutekeleza imani na ibada zake kwa Jehova Mungu muumba wa vyote ambaye ndiye Mungu wetu sote.

Kama Wakristo inatubidi kuangalia mambo ambayo ni muhimu kuyaongeza na mengine kuyapunguza katika katiba yakienda sambamba na yale yanayohitaji maboresho ama marekebisho ili kuweza kuendana na kasi ya maendeleo duniani pasi na kudhuru Ukristo pamoja na masilahi ya Kikristo katika nchi yetu.
 Bwana na wabariki sana; maoni au ushauri mkahaya@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

karibu kutoa maoni | your comments are welcomed